Habari na Matukio

Tarehe: 18/01/2020

WABUNIFU WA MAVAZI NCHINI TANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA KATIKA KUUZA MAVAZI YAO NDANI NA NJE YA NCHINa Mwandishi Wetu

Rai hiyo imetolewa na mbunifu wa mavazi hapo nchini Ally Rehmtulla jumamosi ya tarehe 18/01/2020 katika ufunguzi wa kituo cha kuuza kazi za wabunifu wa mavazi hapa nchini kilichopo barabara ya Chole,Masaki jijini Dar Es Salaam, kwa kushirikiana na kampuni za kutengeneza nguo,Flygle na high-tech wear kutoka nchini china.
Rehmtulla ambaye elimu yake ya fani ya ubunifu wa mavazi aliipata nchini Marekani katika chuo cha The Baum School of Art anasema, kuwepo kwa kituo hiki ni fursa kwa wabunifu wa mavazi kukitumia ili kuonesha pamoja na kuuza kazi zao hasa zile zilizobuniwa hapa nchini na zinazotumia malighafi hususani pamba.
Aidha wabunifu wa mavazi wapatao wanne kutoka Tanzania kwa kuanzia watapata fursa ya kuuza kazi zao kwa kipindi cha miezi mitatu mitatu ili kupisha makundi mengine.Lakini pia amewataka wabunifu wachanga katika fani ya ubunifu wa mavazi kujitokeza kwa wingi katika kuchangamkia fursa za kiuchumi kwani wakati ni sasa.
Naye Bi.Vivian Shalua ambaye ni Afisa Sanaa Mwandamizi kutoka baraza la Sanaa la Taifa(BASATA) amempongeza Ally Rehmtulla kwa kushirikiana na kampuni za kutengeneza vitambaa vya nguo,Flygle na high-tech wear kutoka nchini, kwa kuja na wazo la kuanzisha kituo kitakachokuwa kinaonesha na kuuza kazi mbali mbali za mavazi kutoka tanzania na hivyo kutoa rai kwa vijana hasa wale wanaofanya kazi za ubunifu wa mavazi kubuni pamoja na kushona nguo zitakazotangaza utanzania wetu kujitokeza kwa wingi katika kuzalisha nguo zenye ubora ili ziwe kivutio kwa watumiaji wa mavazi haya.
Uzinduzi huu walihudhuriwa na wasanii mbali mbali akiwemo mwanamitindo maarufu hapa nchini Flaviana Matata ambaye aliwataka wabunifu wa mitindo nchini kuwa kitu kimoja katika kukuza fani hii lakini pia kushirikiana katika mambo mbali mbali ya ubunifu,pamoja na kutafuta masoko,kufanya tafiti zinazohusu fani hii ya mavazi kwani kwa kufanya hivyo watazidi kuitangaza Tanzania kimataifa.

Pamoja na uzinduzi wa kituo hiki kitakachukuwa na jukumu la kuuza nguo zilizobuniwa na wasanii kutoka Tanzania, siku hii pia iliendana na shamra shamra za kusheherekea siku ya kuzaliwa kwa mbunifu wa mavazi,Ally Rehmtulla ambaye alizaliwa tarehe 18/01/1986

Copyright © 2021. All Rights Reserved.