Habari na Matukio

PRESS RELEASE

Tarehe: 12/10/2015

BASATA LAWAPONGEZA WASANII DIAMOND, VANESSA MDEE NA OMMY DIMPOZ KWA KUSHINDA TUZO ZA AFRIMMA
Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) likiwa ni msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linapenda kutoa pongezi za dhati kwa Wasanii wa muziki wa kizazi kipya Nassib Abdul maarufu kama Diamond, Omary Faraji Nyembo maarufu kwa jina la Ommy Dimpoz na Vanessa Mdee maarufu kwa jina la Vee Money kwa kushinda tuzo mbalimbali kwenye Tuzo za African Music Magazine Awards (AFRIMMA) zilizofanyika jijini Dallas nchini Marekani.


Katika tuzo hizo Msanii Diamond ameshinda tuzo tatu ambazo ni Video Bora ya Kucheza (Best Dance Video), Msanii Bora wa Mwaka (Best Artist of the Year) na Msanii Bora wa Kiume wa Afrika Mashariki (Best Male East African Artist). Aidha Ommy Dimpoz na Vanessa Mdee wameshinda tuzo za Best New Artist in Africa (Msanii Bora Mpya Africa) na Msanii Bora wa kike wa Afrika Mashariki (Best Female East African Artist) sawia.


Kuteuliwa kwa wasanii wetu na baadaye kushinda katika tuzo mbalimbali za Afrika na duniani ni ishara kwamba wasanii wetu wanakubalika ndani na nje ya Tanzania na kwamba hawana budi kuhakikisha wanatumia fursa hizi katika kupanua wigo wa fursa za masoko kitaifa na kimataifa.


Baraza linatoa wito kwa wasanii na wadau wote wa muziki kuzidisha ubunifu, nidhamu, bidii, mshikamano na weledi katika kazi wanazozifanya ili wasanii wengi wa Tanzania waweze kuchomoza katika tuzo na majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kulitangaza Taifa na kukuza soko la kazi zao.


Ni matumaini ya Baraza kwamba wasanii wataendelea kutambua umuhimu wa kufanya kazi na mapromota wenye upeo na mapenzi mema, kufuata Sheria, Kanuni na taratibu za kutambuliwa na Serikali na zaidi kuhakikisha wanapokwenda nje ya nchi wanafuata taratibu zote sambamba na kukabidhiwa bendera ya Taifa kama ishara ya uwakilishi wa Taifa letu.


SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI


Godfrey Mngereza

KATIBU MTENDAJI


Copyright © 2021. All Rights Reserved.