TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tarehe: 03/04/2015
BASATA YAPIGA MARUFUKU DISKO TOTO NA UKIUKAJI WA SHERIA ZA UENDESHAJI KUMBI ZA BURUDANI KIPINDI
HIKI CHA SIKUKUU YA PASAKA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani kufuata sheria, kanuni na taratibu walizopewa kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.
Wanaelekezwa kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa utumizi
wa kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua kwenye maeneo maalum hasa makazi ya watu na kuhakikisha ulinzi na
usalama wa maisha ya watu.
Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki wote wa kumbi za burudani kwamba ni marufuku kukusanya watoto katika
kumbi zao kupitia kile kinachoitwa 'Disko Toto' ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.
Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi wamiliki wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kumezwa
na faida katika biashara zao kiasi cha kuandaa madisko ya watoto hali mbayo imekuwa ikisababisha maafa
makubwa ambayo yangedhibitika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.
BASATA kama mtoaji wa vibali vya kumbi za sherehe na burudani linasisistiza kwamba halitafumbia macho ukumbi
wowote utakaokiuka maelekezo haya sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa binadamu
hasa yale yanayoonesha maungo ya ndani. Hatua kali na za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka
maagizo haya.
BASATA linawatakia wasanii na wadau wote wa Sanaa sherehe njema ya Pasaka yenye furaha tele.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI