Habari na Matukio

Tarehe: 14/02/2020

KAZI YA SANAA NI CHANZO MUHIMU KWA WASANII CHA KUJIPATIA KIPATO ENDAPO FANI HII ITAFANYWA KWA KUZINGATIA WELEDI HAPA NCHINI.Na Mwandishi Wetu

Kazi ya sanaa ni mojawapo ya chanzo muhimu cha kujipatia kipato kwa wasanii mbali mbali hapa nchini endapo kazi hii itafanywa kwa kuzingatia weledi zaidi.


Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wa Habari wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC nchini Tanzania Bwana Faraja Samo, ambaye ni mtayarishaji wa kipindi cha Haba na Haba,Katibu Mtendaji wa BASATA,Godfrey Mngereza amesema kuwa, sheria Na.23 ya mwaka 1984,Baraza la Sanaa la Taifa limeainisha Sanaa katika shughuli mbali mbali za Ubunifu kama vile, Uchoraji, Uchongaji, Uhunzi, Ususi, Ufumaji, Ushonaji, Usanifu majengo, pamoja na Upishi wa vyakula mbali mbali.
Pia Katibu Mtendaji wa BASATA,Mngereza amezitaja Sanaa nyingine kuwa ni pamoja na Sanaa ya Tamthilia,Filamu,Muziki wa asili na dansi,Sarakasi,Ngoma,kwaya pamoja na Taarabu,ambapo shughuli zote hizi ni baadhi tu ya kazi zifanywazo na wasanii kwa malipo iwe katika vikundi,vyama,kampuni,Serikali au mtu binafsi.
Utafiti uliofanywa na BASATA katika siku za hivi karibuni,limebaini kuwa kazi za Sanaa zinavyoweza kumuongezea kipato pamoja na kutoa ajira kwa wasanii,kupunguza umasikini na hivyo kutoa taswira iliyojengeka miongoni mwa jamii kwamba Sanaa bado inatizamwa kama sehemu ya Utamaduni na Burudani na siyo chanzo cha ajira na kipato.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2018-2019 inaonyesha kuwa, sekta inayoongoza kwa kuupaisha uchumi wa nchi ni ile ya sanaa na burudani ambayo ilikua kwa asilimia 13.7 ikipiku kasi ya ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo sekta za ujenzi (asilimia 12.9), usafirishaji (asilimia 11.8), sayansi na elimu ya ufundi (asilimia 9.9) na hata habari na mawasiliano (asilimia 9.1). Swali la kujiuliza kwa wasanii wasanii wetu nchini Tanzania ni kwamba,Je? wanatambua na kunufaika kikamilifu kutokana na nguvu hii kubwa ya kiuchumi waliyonayo? Wanaziona fursa? Wanazitumia? Ni wazi kuwa kwa kutokuziona na kuzitumia fursa hizo kikamilifu, wasanii, kama walivyo wanajamii wengine wasioweza kuona fursa mbalimbali zinazowazunguka wataendelea kutumika kama nyenzo za kuwanufaisha na kuwatajirisha wengine.
Kwa mantiki hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa,Godfrey Mngereza kupitia kipindi cha Haba na Haba cha Idhaa ya Kiswahili ya BBC, amewashauri wasanii kote nchini kuzingatia taaluma zao kwa maana ya kuwa makini katika suala zima la kuingia mikataba na wafanyabiashara wa kazi za sanaa, kujielimisha zaidi katika fani zao hususani katika nyanja ya ubunifu lakini pia kuzingatia ubora wa kazi wanazozizalisha, na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejiongeza kipato kupitia kazi zao za Sanaa.
Copyright © 2021. All Rights Reserved.