Habari na Matukio

PRESS RELEASE

Tarehe: 05/11/2015

BASATA KUWAKUTANISHA WASANII KUIJADILI SIKU YA MSANII
Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ijumaa hii ya tarehe 06/11/2015 linatarajia kuyakutanisha mashirikisho na vyama vya wasanii nchini kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam ili kuweka mikakati ya pamoja katika kufanikisha siku ya msanii maarufu kama Msanii Day inayotarajiwa kufanyika tarehe 12/12/2015.


Kwa mujibu wa Mratibu wa Siku ya Msanii kutoka Kampuni mwendeshaji wa siku ya Msanii (Msanii Day) Haakneel Production Tanzania (LTD) Bw. Justine Kusaga lengo la kuwakutanisha wasanii ni kuwa na mjadala wa pamoja ili kuhakikisha siku hii ya Msanii inafanyika kwa mafanikio makubwa na kuwafanya wasanii wote kuwa sehemu ya siku hii muhimu kwao.


“Haakneel kwa kushirikiana na BASATA ambao ni wamiliki wa mradi huu wa siku ya msanii tumeamua kuwaita wasanii kupitia mashirikisho na vyama vyao ili kuhakikisha kila msanii anakuwa sehemu ya maadhimisho ya siku hii muhimu lakini pia kuifanya siku hii kuwa yenye mafanikio” alisema Kusaga.


Alizidi kueleza kwamba, mwaka huu siku ya msanii imepangwa kuwa ya tofauti ambapo shamrashamra zake zimepangwa kuanza mapema zaidi kwa kuhusisha shughuli na matukio mbalimbali ya kisanaa kabla ya kilele ambacho kinatarajiwa kupambwa na burudani mbalimbali za Wasanii.


“Tunawaita wasanii Ijumaa hii ili kwa pamoja tujadiliane, tuweke mikakati ya pamoja na kuhakikisha kunakuwa na shamrashamra nyingi za wasanii ambazo zitawafanya waimiliki siku hii maana hakika siku hii ni yao wasanii” alisisitiza Kusaga.


Siku ya Msanii maarufu kama Msanii Day ni mradi unaomilikiwa na BASATA ambao lengo lake ni kuenzi, kuthamini na kutambua michango mbalimbali ya wasanii nchini na kwa mara ya kwanza iliazimishwa tarehe 25 Oktoba mwaka jana wa 2014


IMETOLEWA NA KITENDO CHA HABARI NA MAWASILIANO, BASATA


Copyright © 2021. All Rights Reserved.