Habari na Matukio

PRESS RELEASE

Tarehe: 17/02/2016

BASATA LAMPONGEZA MSANII JOSEPH STANFORD ALIYETEMBEA KWA MIGUU KUTOKA MWANZA HADI DAR ES SALAAM KUMPONGEZA RAIS MAGUFULI
Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limempongeza Msanii Joseph Stanford kutoka Mwanza aliyetembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa 1200 kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na utendaji wake pia uundaji wa Idara ya Sanaa iliyo chini ya Wizara ya Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni.


Aidha, BASATA imempa zawadi ya usajili bure msanii huyu ili atambuliwe rasmi katika tasnia ya Sanaa na baadaye kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za sekta hii.


Akizungumza ofisini kwake, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza alisema kuwa Stanford ameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yake kwani haikuwa kazi rahisi kutembea umbali mrefu na usiku na mchana kuja kumpongeza Rais Dkt. Magufuli.


“Sisi kama Baraza tunafarijika sana, tunafurahi kuona wasanii na vijana kwa ujumla mnakuwa wazalendo na kufurahishwa na kasi ya utendaji wa Serikali ya awamu ya tano. Tunafurahi zaidi unapopeleka ujumbe wa Wasanii kwamba wamefurahia kuundwa kwa idara ya Sanaa” alisema.


Aliongeza kuwa BASATA limetambua uzalendo na moyo wake wa kuipenda Sanaa hivyo limeamua kumpa zawadi ya usajili bure ili iwe chachu ya kujikita kwenye Sanaa na kufanya kazi zake kwa weledi na kuzingatia maadili ya kitanzania.


Kwa upande wake kijana Stanford alisema kwamba anafurahia kwa mapokezi aliyopewa na BASATA huku akisisitiza kuwa ndoto yake ni kumfikishia salamu za pongezi Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli lakini pia kupata mafanikio kwenye kazi za Sanaa.


“Nafurahi sana kwa mapokezi niliyopata, muda wowote nitaenda kumfikishia salamu za pongezi Rais wangu. Matumaini yangu ni kuona sekta ya Sanaa inazidi kuthaminiwa na kusonga mbele” alisisitiza Stanford.


Msanii Stanford anatokea eneo la Mabatini jijini Mwanza na ametembea kwa siku ishirini na tano kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam na ametumia kiasi cha shilingi elfu arobaini na tano pekee.


Hata hivyo, alizitaja changamoto mbalimbali zinazolikabili Baraza hilo kuwa ni pamoja na kutokukamilika kwa Ukumbi wa maonesho ulioanza kujengwa BASATA toka mwaka 2006, siasa kuingilia utendaji kwenye sekta ya Sanaa, kupitwa na wakati kwa sheria na kanuni za BASATA na kutokuwepo kwa sera inayosimamia Sanaa moja kwa moja.


Katibu Mkuu Profesa Elisante Ole Gabriel aliteuliwa rasmi kushika wadhifa huo Oktoba 23 mwaka 2015 na wiki hii nzima amekuwa katika vikaokazi na ziara katika taasisi na idara zote zilizo chini ya wizara yake.


Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)Copyright © 2021. All Rights Reserved.