Habari na Matukio

PRESS RELEASE

Tarehe: 24/02/2016

BASATA YAONYA WASANII DHIDI YA MATAPELI
Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote kuwa makini na wakuzaji Sanaa (Mapromota) au baadhi ya wanaojiita wadau wa Sanaa ambao wamekuwa wakitumia njia za kiulaghai na utapeli katika kujipatia faida na manufaa kupitia mgongo wa Wasanii.


Baraza linatoa angalizo hili kufuatia kuwepo kwa ongezeko la matukio ya baadhi ya watu wanaojiita wadau wa Sanaa ambao wamekuwa wakiwadanganya wasanii na kuwalaghai kwa kuwaahidi fursa mbalimbali kama za maonesho ya ndani na nje ya nchi ambazo hata hivyo zimekuwa zikiishia katika kuwaletea wasanii matatizo kiuchumi na kijamii.


Aidha, watu hao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi wa Serikali kuwatapaeli wasanii na kujipatia fedha isivyo halali.


BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwamba kabla hawajaingia makubaliano yoyote na mtu, asasi au kampuni yoyote wawasiliane na wanasheria au watoe taarifa Ofisi za Utamaduni za wilaya au manispaa zilizo karibu nao ili kuhakikisha wanaepuka ulaghai na udanganyifu kutoka kwa watu hao wasio waaminifu.


Aidha, kwa wasanii walioko Dar es Salaam BASATA linawaelekeza kufika Ofisi zake zilizoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Slaam ili wapate msaada wa kisheria na kujiridhisha kama makubaliano yao ni halali na ya uhakika.


Mwisho kabisa, BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwa ujumla kwamba, tangu Januari Mosi mwaka 2013 tasbia za muziki na filamu ni rasmi hivyo Wasanii wote hawana budi kusajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na wanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za uendeshaji wa kazi za Sanaa nchini.


Aidha, kila msanii anawajibika kuhakikisha anafanya kazi na mtu, watu, asasi au kampuni iliyo na vibali halali vya kuendesha shughuli za Sanaa na si vinginevyo.


SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI


GODFREY L. MNGEREZA

KATIBU MTENDAJI - BASATACopyright © 2021. All Rights Reserved.