Habari na Matukio

PRESS RELEASE

Tarehe: 07/03/2016

BASATA YAWAPONGEZA WASANII LULU NA RICH RICH KUSHINDA TUZO ZA AMVCA 2016
Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kama msimamizi na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linapenda kutoa pongezi za dhati kwa Wasanii Singo Mtambalike (Rich Rich) na Elizabeth Michael (Lulu) kwa kushinda tuzo za African Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA2016) zilizotolewa mwishoni mwa wiki nchini Nigeria na kushuhudiwa na Dunia kupitia luninga na mitandao ya kijamii.


Katika tuzo hizo Msanii Singo Mtambalike ameshinda tuzo ya Filamu Bora ya Lugha ya Asili (Best Local Language - Swahili) kupitia filamu ya ‘Kitendawali’ huku Msanii Elizabeth Michael (Lulu) akishinda tuzo ya Filamu Bora ya Afrika Mashariki (Best Movie -Eastern Africa) kupitia filamu yake ya 'Mapenzi'.


Kuteuliwa na kushinda kwa Wasanii wa Tanzania katika tuzo hizi zilizoshirikisha wasanii na filamu nyingi za Afrika ni ishara kwamba wasanii wetu wanakubalika, kutambuliwa na kuthaminiwa ndani na nje ya Tanzania.


Aidha, ushindi huu unazidi kulipa heshima na kulitangaza taifa letu katika nyanja mbalimbali hivyo kuzidi kulifanya ling’ae na kuwa kinara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.


Baraza linatoa wito kwa wasanii na wadau wote kuzidisha ubunifu, bidii na weledi katika kazi wanazozifanya ili wasanii wengi zaidi waweze kuchomoza katika tuzo na majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa lengo la kulitangaza taifa na kukuza soko la kazi zao kimataifa.


Ni matumaini ya Baraza kwamba wasanii wataendelea kutambua umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu za kutambuliwa na Serikali.


SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI


GODFREY L. MNGEREZA

KATIBU MTENDAJI - BASATACopyright © 2021. All Rights Reserved.