Habari na Matukio

TANGAZO KWA WASANII WOTE NA VYOMBO VYA HABARI

Tarehe: 13/04/2017

BASATA LAPIGA MARUFUKU DISCO TOTO, KUMBI ZISIZO NA VIBALI.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini limepiga marufuku kumbi zote za burudani zisizo na vibali kufanya maonesho ya aina yoyote.


Aidha, BASATA linawakumbusha wamiliki na waendeshaji wa kumbi za burudani wenye vibali kufuata Sheria, Kanuni na taratibu zilozopo kwenye vibali vyao vya uendeshaji wa kumbi.


BASATA linawaelekeza wamiliki na mameneja wa Kumbi zote nchini kuhakikisha wanakuwa na vibali halali vya uendeshaji wa kumbi zao, kuzingatia muda wa matumizi ya kumbi, kuepuka kelele zinazosumbua wanajamii hasa katika makazi ya watu na pia wahakikishe wanatoa ushirikiano katika mamlaka zinazosimamia ulinzi na usalama wa watu na mali zao.


Aidha ni marufuku kukusanya watoto katika kumbi kupitia kile kinachoitwa ‘Disko Toto’. Wazazi tuhakikishe kuwa watoto wetu wanakuwa salama katika kipindi hiki cha sikukuu kwa kutowaruhusu kushiriki katika shughuli ambazo zinaweza kuwapeleka kufikwa na maafa au madhara mengineyo.


Uzoefu unaonesha kwamba, nyakati za sikukuu kama hizi za Pasaka baadhi ya wamiliki na mameneja wa kumbi wamekuwa wakijisahau na kumezwa kwa kutengeneza faida katika biashara zao kiasi cha kuandaa "Disco Toto" hali ambayo imekuwa ikisababisha madhara ambayo yangeweza kuepukwa kwa kufuata Sheria za nchi.


BASATA linasisistiza kwamba halitafumbia macho ukumbi wowote utakaokiuka masharti ya usajili sambamba na kuruhusu maonesho machafu yenye kudhalilisha utu wa mtu.


Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya.


Baraza la Sanaa la Taifa linawatakia wasanii, wadau wa Sanaa na Watanzania wote sherehe njema ya Pasaka na yenye furaha tele.


Sanaa ni kazi, tuipende na kuithaminiGODFREY MNGEREZA


KATIBU MTENDAJI


Copyright © 2021. All Rights Reserved.