Habari na Matukio

Tarehe: 12/02/2020

HATIMAYE MSANII WA BONGO FLEVA GODFREY TUMAINI (DUDU BAYA) APATA KIBALI CHA KUENDELEA NA KAZI YAKE YA SANAA YA MUZIKINa Mwandishi Wetu

Mwanamuziki wa Bogo Flava Godfrey Tumaini maarufu Dudu Baya hatimaye ameruhusiwa kuendelea na kazi yake ya Muziki kufuatia Baraza la Sanaa la Tafa(BASATA) kumfutia usajili wake baada ya kukiuka maadili ya kazi za Sanaa hapa nchini.


Mnamo tarehe 6/01/2020 Msanii Dudu Baya alikaidi wito alioitwa na BASATA ili kutoa maelezo kuhusu tuhuma zilizokuwa zinamkabili na hivyo kutafsiriwa kuwa ni dharau kwa Baraza.Hata hivyo baada ya siku kadhaa msanii huyu aliamua kuja Basata kwa ajili kuomba radhi na kutoa maelezo kuhusu tuhuma ambazo BASATA walimwandikia barua.
Aidha BASATA walimshauri Msanii Godfrey Tumaini kukata rufaa kwa waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Mwakyembe endapo anaona kwamba hakutendewa haki.


Kufuatia sakata hili, Dkt.Harrison Mwakyembe alimuita Dudu Baya ambaye pamoja na kumsikiliza kwa kina hatimaye alimuondolea adhabu ya kufungiwa na BASATA kutojishughulisha na kazi ya Sanaa.Waziri alimtaka yeye pamoja na Wasanii wengine kote nchini hususani Muziki wa kizazi kipya kufuata sheria,kanuni pamoja na taratibu zilizowekwa na serikali huku Baraza la Sanaa la taifa likiwa ndilo msimamizi Mkuu wa Sanaa hapa nchini.
Dkt. Mwakyembe alisisitiza kuwa, Taifa la Tanzania halipo tayari kuendesha kazi zake za Sanaa kinyume na taratibu za nchi, kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaliangamiza taifa ambalo wengi wao ni vijana.


Naye Katibu mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza aliiwakumbusha wasanii akiwemo Mwanamuziki wa Bogo Flava Godfrey Tumaini maarufu Dudu Baya kuwa, BASATA kama msimamizi wa sekta ya Sanaa nchini wataendelea kusimamia kazi za sanaa na wasanii wote kwa kujenga maadili mema kwa wasanii,huku wakikumbuka kuwa Sanaa ni kazi,na wasanii ni kioo cha jamii hivyo pale wanapokosea jukumu la Baraza ni kuwarekebisha pamoja na kutoa elimu sahihi ya sanaa inayolenga mila na desturi za taifa letu la Tanzania.
Kwa upande wake Msanii Godfrey Tumaini maarufu Dudu Baya amemshukuru Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Mwakyembe kwa ushauri wake mzuri na kuahidi kuyazingatia mambo yote aliyomshauri na kwamba atakuwa msanii mhamasishaji wa maadili mema kwa wasanii ili Tanzania iweze kupiga hatua kimataifa kupitia muziki ikiwa ni pamoja na kutangaza vyema lugha yetu ya Kiswahili na kwamba atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vyote vinavyojihusisha na sanaa hapa nchini hususani Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
Copyright © 2021. All Rights Reserved.