Habari na Matukio

PRESS RELEASE

Tarehe: 13/11/2015

PROFESA ELISANTE AIPONGEZA BASATA KWA UTENDAJI KAZI, ATAKA JUHUDI ZAIDI
Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel amelipongeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa mafanikio yake katika kuratibu na kuisimamia sekta ya Sanaa nchini huku akitaka juhudi zaidi ziongezwe katika maeneo ya kuwatafutia wasanii masoko.


Akizungumza mwishoni mwa wiki hii (siku ya AlhamisI) wakati alipofanya ziara maalum makao makuu ya BASATA Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam Profesa Elisante alisema kuwa moja ya sifa kuu ya BASATA ni kusimamia sheria, kanuni na taratibu katika kuhakikisha sekta ya Sanaa inakuwa na maadili pia utaratibu katika uendeshwaji wake.


“Nimefurahi mnafanya kazi vizuri. Moja ya sifa kubwa mliyonayo ni kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu pamoja na changamoto mbalimbali mnazokumbana nazo” alisema Profesa Elisante.


Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio yanayopatikana kwenye sekta ya Sanaa na kazi nzuri inayofanywa na BASATA bado kuna changamoto kadhaa hasa katika eneo la upatikanaji wa masoko ya uhakika ya kazi za wasanii na kwamba hili ni eneo ambalo BASATA halina budi kulitazama kwa umakini.


“Ni lazima tuhakikishe tunawapa Wasanii uhakika wa masoko ya kazi zao. Nina amini kuna kazi nyingi sana za wasanii hazijulikani vizuri na hazijawekewa mkakati maalum wa masoko. Kazi ya BASATA iwe ni kuhakikisha wasanii wanazalisha kazi bora, wanapata mahali pa kuuza kazi na kwa bei nzuri” aliongeza Profesa Elisante.


Kuhusu utendaji, alisisitiza kwamba katika awamu hii ya serikali ya tano lazima BASATA ifanye kazi kwa kasi ili kwenda sambamba na kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya Hapa Kazi Tu na kuhakikisha kunakuwa na ubunifu, heshima, uadilifu, uzalendo na uzingatiaji sheria na miongozo mbalimbali mahali pa kazi.


Awali akimkaribisha Katibu Mkuu, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza alitaja mafanikio mbalimbali ya Baraza hilo kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa siku ya msanii, tuzo za muziki, programu za sanaa kwa watoto, mafunzo ya stadi za Sanaa kwa wasanii na viongozi wao, programu ya Jukwaa la Sanaa na mafanikio mengine mengi.


“Mheshimiwa Katibu Mkuu, Baraza limefanikiwa pia kuwakutanisha wasanii na mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii kama NSSF, GEPF, PPF na moja ya mafanikio ya hivi karibuni ni wasanii zaidi ya ishirini na wanane (28) kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)” alisisitiza Mngereza.


Hata hivyo, alizitaja changamoto mbalimbali zinazolikabili Baraza hilo kuwa ni pamoja na kutokukamilika kwa Ukumbi wa maonesho ulioanza kujengwa BASATA toka mwaka 2006, siasa kuingilia utendaji kwenye sekta ya Sanaa, kupitwa na wakati kwa sheria na kanuni za BASATA na kutokuwepo kwa sera inayosimamia Sanaa moja kwa moja.


Katibu Mkuu Profesa Elisante Ole Gabriel aliteuliwa rasmi kushika wadhifa huo Oktoba 23 mwaka 2015 na wiki hii nzima amekuwa katika vikaokazi na ziara katika taasisi na idara zote zilizo chini ya wizara yake.


Imeandaliwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha


Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)

Copyright © 2021. All Rights Reserved.