Habari na Matukio

Tarehe: 10/03/2020

ZIARA YA KATIBU MKUU WA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO DKT. HASSAN ABBAS MAKAO MAKUU YA BASATA JIJINI DAR ES SALAAM.Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo,Dkt.Hassan Abbas amewakumbusha Menejimenti pamoja na Wafanyakazi wa Baraza Sanaa la Taifa(BASATA) kwamba, kama kweli wanataka kufikia matarajio waliyojiwekea jambo la muhimu ni kuwa Wachapa kazi,Waadilifu na Wazalendo ndani ya Wizara na Serikali lakini pia kuwa wabunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.


Rai hiyo ameitoa tarehe 20/03/2020, makao Makuu ya BASATA- Ilala Shariff Shamba jijini Dar Es Salaam alipokutana na Menejimenti ya Baraza la Sanaa la Taifa katika utaratibu wake wa kutembelea taasisi zilizopo ndani ya Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,ili kuona mafanikio pamoja na changamoto zilizopo ndani taasisi hizo na hatimaye kuzitafutia suluhisho ya changamoto hizo.
Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbas amewakumbusha wafanyakazi wa BASATA kuwa, Sanaa inakuwa na kwamba ni kama chakula cha roho na kwa kutambua hilo,BASATA wanajukumu la kukuza na kuendeleza sanaa hiyo hapa nchini kwa kuzingatia kanuni na sheria za nchi.


Aidha, katika kutekeleza majukumu ya Baraza, Katibu Mkuu,Dkt. Hassan Abbas pia ameishauri menejimenti ya BASATA kubuni zaidi vyanzo mbali mbali vya mapato kama njia mojawapo wa kupanua wigo wa kuongeza kipato ndani ya Baraza tofauti na hivi sasa ambapo vyanzo vikuu vya mapato vinatokana na ada za vibali,kodi za majengo,ufadhili pamoja na misaada toka kwa wadau mbali mbali.
Suala la ushirikiano sehemu ya kazi kati ya Menejimenti pamoja na wafanyakazi ni eneo jingine ambalo Dkt.Abbas amesisitiza kwani ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo sehemu ya kazi,lakini pia akiwakumbusha wafanyakazi kujiendeleza kitaaluma kwani teknolojia kwa hivi sasa inakua kwa kasi na Wasanii wanahitaji kupata maarifa mapya ya kazi za Sanaa,hivyo wafanyakazi waliopewa dhamana hiyo wanapaswa kujiendeleza zaidi ili kuendana na hali halisi ya ukuaji wa sayansi na teknolojia ikiwemo sekta ya Sanaa.


Kabla ya kuhitimisha ziara yake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Dkt.Hassan Abbas akiongozana na Katibu Mtendaji wa BASATA,Bw.Godfrey Mngereza alipata fursa ya kutembelea mradi wa ukumbi wa maonesho ya Sanaa wa Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA)jengo ambalo limesimama kwa hivi sasa kutokana na ukosefu wa fedha za kuendeleza mradi huu.
Copyright © 2021. All Rights Reserved.