Habari na Matukio

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MSANII CHIJWELE CHE MUNDUGWAO

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Msanii wa muziki wa asili Chijwele Chemundugwao kilichotokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam leo mapema Asubuhi ya Alhamisi ya tarehe 16/04/2015 baada ya kuugua kwa muda mrefu.


Che mundugwao ni msanii wa muziki wa asili na mdau wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa na mchango mkubwa katika kukuza muziki wa asili nchini na baadaye kupitia Chama cha Muziki wa asili (TAFOMA) nchini alishiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uanzishwaji wa Shirikisho la Muziki ambalo linaviunganisha vyama vya wasanii wanamuziki nchini.


Mchango wake katika muziki wa asili na katika kujenga mfumo wa utawala wa wasanii nchini hautasahaulika kamwe. Ni mdau aliyeacha misingi katika sekta ya muziki na amejitolea kwa kiasi kikubwa katika kuufikisha muziki huu mahali ulipo leo.


Baraza, wasanii na wadau wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote aliyotuachia marehemu Che mundugwao hasa katika kupenda kujitolea muda mwingi kufanikisha ufanisi kwenye sekta ya Sanaa.


Baraza linatoa pole kwa ndugu wa marehemu, shirikisho la muziki, wasanii na wadau wote wa Sanaa kwa msiba huu.Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Amen


Godfrey Mngereza

KATIBU MTENDAJI

Copyright © 2021. All Rights Reserved.