Habari na Matukio

TANGAZO KWA WASANII WOTE NA VYOMBO VYA HABARI

Tarehe: 17/08/2015

PAUL MAKONDA AIPONGEZA BASATA KWA KUJALI AFYA ZA WASANII
Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ndugu Paul Makonda amelipongeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kujali afya za wasanii kufuatia kuandaa semina maalum kwa ajili ya kuwaelimisha wasanii umuhimu wa kuwa na bima ya afya.


Akizungumza mwishoni mwa wiki hii kwenye ufunguzi wa semina hiyo ya siku moja iliyofanyika kwenye Ukumbi mpya wa Baraza hilo ulioko Ilala Sharif Shamba, Makonda alisema kuwa pamoja na BASATA kuratibu sekta ya Sanaa limeona ni vema wasanii kulinda afya zao na kuhakikisha wanakuwa na afya njema kupitia kuwa na bima ya afya.


"Nawapongeza sana BASATA kwa kuona umuhimu wa afya kwa wasanii wetu. Kumbe pamoja na kuratibu sekta ya Sanaa na kukusanya mapato kutoka kwenye kazi za Sanaa BASATA wanauona umuhimu wa afya kwa wasanii" alisema Makonda


Aliongeza kwamba katika siku za hivi karibuni wasanii wamekuwa wakiombaomba fedha kwa ajili ya matibabu ama kutatua matatizo mbalimbali hali ambayo inatokana na wao kutojiwekea akiba ya fedha ili iweze kufaa katika kutatua changamoto hizo.


"Ni fedheha kubwa kwa wasanii tena wengine maarufu kuombaomba kwa ajili ya matibabu. Lazima watokane na aibu hii kwa kujiwekea akiba ya fedha kupitia mfuko wa Bima ya afya. Hili litamaliza kabisa tatizo la wasanii kukosa fedha za matibabu" alisema Makonda.


Aidha, Makonda alieleza kushangazwa na kukosekana kwa wasanii wengi maarufu kwenye semina hiyo na kueleza kwamba wao ndiyo wamekuwa ombaomba wakubwa pale wanapokuwa na shida ya matibabu na wengine wamefikia hatua ya kuomba hata fedha za pango.


"Nashangaa sana katika semina hii muhimu baadhi ya wasanii wakubwa siwaoni. Wanajiona wakubwa lakini wao ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kuombaomba pale wanapokuwa na tatizo la matibabu na hata kodi za nyumba wanazoishi" alieleza Makonda.


Awali akimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya, Katibu Mtendaji wa BASATA Ndugu Godfrey Mngereza alisema kwamba BASATA limeandaa semina hiyo kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) baada ya kuona wasanii wamekuwa na tatizo la kugharamia matibabu na wamekuwa ni wa kutembeza bakuli pale wanapougua.
Copyright © 2021. All Rights Reserved.