Habari na Matukio

Tarehe: 22/10/2019

TATHIMINI YA SHINDANO LA MISS TANZANIA 2019Na Mwandishi Wetu

Muandaaji wa Mashindano ya ulimbwende ya Miss Tanzania Basila Mwanukuzi kupitia kampuni yake The Look ameiambia BASATA kuwa shindano lake la mwaka huu la Miss Tanzania 2019 limefanikiwa kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na Mwaka uliopita. Akizungumza na kamati ya Tathimini ya BASATA iliyokuwa na jukumu la kuratibu shindano la Miss Tanzania 2019 Mkurugenzi wa The Look,Basila anasema Mashindano hayo yamekuwa yakiyumba kwa miaka kadhaa lakini mwaka huu kumekuwa na mwamko wa kipekee.
Aidha mojawapo ya Changamoto zilizojitokeza katika shindano la mwaka huu ni pamoja na kukosekana kwa wadhamini wa kutosha, Bi Mwanukuzi anaamini mwakani wadhamini watajitokeza kwa wingi na kuyarudisha kwenye umaarufu wake wa awali na ni fursa muhimu kwake na kwa walimbwende wengine wanaohitaji fursa hiyo. Bi. Mwanukuzi ambaye pia ni mshindi wa mashindano hayo mwaka 1998 amesema licha ya changamoto zilizokuwepo malengo yake ni kuendelea kupeperusha bendera ya Miss Tanzania.
Kwa upande wao BASATA,wametumia kikao hiki cha Tathimini kumpongeza Mwanukuzi kwa kufanikisha shindano la Miss Tanzania 2019 na kumtaka aboreshe zaidi shindano hili kwa kutoa elimu zaidi inayohusu fani ya Ulimbwende kwa waandaji pamoja na washiriki wa Miss Tanzania.


Naye Mshindi wa Miss Tanzania 2019. Silvia Sebastian ambaye awali alitwaa taji la Miss Mwanza na kufanikiwa kuiwakilisha Kanda ya Ziwa katika mashindano ya unyange Miss Tanzania 2019,amesema amelizika na mchakato mzima wa kumpata mshindi na kwamba taratibu zote za mashindano zilizigatiwa na kuondoa dhana ya kwamba washindi wa Ulimbwende uchanguliwa kwa Upendeleo.


Silvia Sebastian aliibuka mshindi wa Miss Tanzania 2019 Agosti 24,2019 katika Ukumbi wa Kisena Millenium Tower jijini Dar Es Salaam na kuhudhuriwa na watu mbali mbali,taasisi(BASATA) akiwemo pia Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa Mgeni Rasmi. Ushindi wa Miss Tanzania 2019,unamfanya sasa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World 2019.


Aidha baada ya kukabidhiwa tuzo yake ya ushindi na kujinyakulia kitita cha shillingi million 10 kama mshindi wa kwanza, Silvia alipata fursa ya kukutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dodoma na kutoa shukurani zake kwa serikali ya Tanzania ya awamu tano kwa jinsi wanavyodumisha nakuthamini Utamaduni wa Mtanzania ikiwemo fani ya Urembo.


Copyright © 2021. All Rights Reserved.