Habari na Matukio

TANGAZO KWA WASANII WOTE NA VYOMBO VYA HABARI

Tarehe: 01/09/2015

MWASITI AWATAKA WASANII WABADILIKE, WAZINGATIE MAADILI WAWAPO JUKWAANI
Na Mwandishi Wetu

Msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya Mwasiti Almas amewataka wasanii wenzake kuwa wabunifu katika kutanua mianya ya kujiingizia kipato na kuhakikisha wanazingatia maadili wawapo jukwaani ili kulinda hadhi zao.


Mwasiti ameyasema hayo mapema wiki hii wakati akijibu maswali ya wadau wa Jukwaa la Sanaa linalofanyika kwa mwezi mara mbili ziku za Jumatatu makao ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ilala Sharif Shamba.


"Wasanii wengi wanang'ang'ania kwenye sanaa pekee. Hawawekezi kwenye miradi mingine. Kuwa na umaarufu si kuwa na fedha bali umaarufu ni njia tu inayokusaidia kuingia kwenye sekta na miradi mbalimbali kwa ajili ya kujiimarisha kimapato" alisema Mwasiti wakati akifafanua suala la wasanii kufilisika mara wanapochuja kwenye Sanaa.


Alizidi kueleza kwamba wasanii waliopo sasa hawana budi kutambua kwamba hawatakuwepo muda wote bali kuna leo na kesho hivyo lazima kuiandaa kesho sasa.


"Umri wa wasanii unaenda, waliopo sasa hawawezi kuwepo kesho kwani kuna wasanii wengi wanaibuka na lazima wapate nafasi. Ni muhimu sana kwa wasanii kuliona hili. Huko nyuma kaka na dada zetu walipata shida ilikuwa ngumu lakini kwa sasa wasanii tunapata kipato na baadhi wanajitahidi kuwekeza" alisema Mwasiti.


Kuhusu wasanii kufanya maonesho yasiyo na maadili, Mwasiti alisema kwamba inasikitisha sana kwani katika hali ya kawaida msanii anayejitambua na kuthamini utu na hadhi yake hawezi akafanya maonesho ya uchi kwani matendo ya wasanii huathiri sana jamii inayowazunguka.


"Matendo yetu wasanii huathiri sana jamii inayotuzunguka. Sisi ni binadamu na tuna leo na kesho. Sipendi siku zijazo watoto wetu waje kuuliza na kushangaa yale tuyafanyayo sasa maana yataendelea kuonekana" alisema Mwasiti.


Katika Jukwaa hilo BASATA lilimwalika Mwasiti na wa msanii mwenzake wa kike Princes Dalyna anayefanya muziki wa reggae ili kueleza historia, changamoto na mafanikio waliyoyapata katika kazi zao za Sanaa.


Copyright © 2021. All Rights Reserved.