TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MHESHIMIWA CAPTAIN JOHN DAMIAN KOMBA (MB)
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Mbunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Captain John Damian Komba kilichotokea jioni ya Jumamosi ya
tarehe 28/02/2015.
Captain John Damian Komba ni msanii na mdau wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa ni taa na
nuru ambayo katika kipindi chote cha uhai wake imeangaza na kutoa mwanga angavu kwenye sekta ya Sanaa.
Mchango wake katika muziki wa dansi, kwaya na ule wa kiweledi katika kuandaa na kukuza wasanii mbalimbali
nchini hautasahaulika kamwe. Ni mdau aliyeacha alama kuu katika muziki wa bendi, kwaya na taarabu na
amejitolea kwa kiasi kikubwa katika kuufikisha muziki wa dansi na kwaya mahali ulipo leo.
Aidha, pamoja na kujiunga na siasa na hatimaye kuwa Mbunge wa jimbo la Mbinga Magharibi, Mheshimiwa Komba
hakukoma kuendelea kuipigania sekta ya Sanaa kwani alikuwa ni mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya
Maendeleo ya Jamii ambayo kwa mujibu wa kanuni za Bunge ndiyo inayoisimamia na kuishauri Serikali katika
masuala yote yahusuyo sekta ya Sanaa na Utamaduni.
Baraza, wasanii na wadau wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote aliyotuachia marehemu John
Komba hasa katika kutunga nyimbo za hamasa na ujumbe makini na wenye mashiko kwa jamii yote ya Watanzania.
Hakika pengo lililoachwa na Marehemu haliwezi kuzibika, kwani imekuwa ni kama mshumaa uliyozimika ghafla
wakati tukiingia kwenye giza.
Baraza linatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Anne Makinda, wabunge
na wadau wote wa Sanaa hususan wasanii kwa msiba huu. Ni matumaini ya Baraza kwamba, tutaendelea kuenzi
mema yote yaliyotendwa na Marehemu, hasa kudumisha upendo na amani katika tasnia yetu ya Sanaa na taifa
kwa ujumla.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, Amen
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI