Habari na Matukio

Tarehe: 05/06/2020

SHAIRI: ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI

Ulikuja duniani, kwa mwendo wa kufichama,
Ikawa kama utani, kutupiana lawama,
Tukajua si utani, vifo viliporindima,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Nenda kafilie mbali, corona tusha kujua,
Huna chako mkatili, tumekwisha kugundua,
Unaleta homa kali, kichwa, mapafu, mafua,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Ulianzia uchina, ukafanya mauaji,
Utaliano tumeona, huko kote mauaji,
Marekani kila kona, Umefanya mauaji,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Kama vile haitoshi, ukaja kwetu Corona,
Wala hatuna ubishi, umetupata Corona,
Siyo kwa wetu utashi, umetuua Corona,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Ukaja kwetu Corona, Africa kutukatili,
Tulijiswali Corona, hofu ikatakabali,
Umefanyiza uchina, na kwa wote majabali
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Kufuru kubwa kwa Mungu, kusema hakuna dawa,
Wakati mwenyezi Mungu, kashusha mimea dawa,
Katupendelea Mungu, Africa tumejaliwa,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Kinga yangu barakoa, na kiwiko kinga kwangu,
Kila ninapokohoa, nitavaa kinga yangu,
Nikipiga chafya poa, nimevaa kinga yangu,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Tukihisi homa kali, mapafu, kichwa, mafua,
Tutenda hospitali, huko watatuagua,
Tahadhari ni dalili, kwamba tumeshakujua
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Kongole nyingi twatoa, kw Rais Magufuli,
Msimamo ulotoa, wewe kweli ni jabali,
Sitafunga ulitoa, hiyo ndo yako kauli,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Pia tunampongeza, Waziri wetu wa Afya,
Ummy Mwalimu kaweza, kuzilinda zetu afya,
Pambano mmeliza, Mabingwa wetu wa afya,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.


Nyote twawapeni pole, mlofikwa na misiba,
Tuwape wote kongole, ninyi mlopata tiba,
Yangu tamati nilale, hadharini kwa akiba,
ONDOKA ZAKO CORONA NENDA KAFILIE MBALI.
HAKI ZA UBUNIFU WA SHAIRI HILI:


Mtunzi: Francis Kaswahili Kaguna
Maneno: Francis Kaswahili Kaguna
Mpangilio: Francis Kaswahili Kaguna
Mgani: Francis Kaswahili Kaguna
Mwaka: 2020.


Copyright © 2021. All Rights Reserved.