Habari na Matukio


Tarehe: 30/04/2014

BASATA, TCRA WATAKA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO YA KIJAMII KWA WASANII


Na Mwandishi Wetu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) mapema wiki hii wamelaani matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii miongoni mwa wasanii wakati wa programu ya Jukwaa la Sanaa iliyofanyika makao makuu ya Baraza hilo yaliyoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.Akiongea wakati akiwasilisha mada iliyohusu 'Matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kwa wasanii', Meneja mawasiliano wa TCRA Innocent Mungy alisema kuwa wasanii ni kioo cha jamii hivyo kwa namna yoyote ile hawapaswi kuwa sehemu ya uharibifu wa jamii inayowazunguka au kuharibu wajihi (taswira) yao kwa jamii yao."Unapokuwa kioo cha jamii, unategemewa kuishi kwa kuwa mfano katika jamii yako. Vijana wengi wanaiga kutoka kwa wasanii ambao ni maarufu. Tunatarajia wasanii wawe mfano kwao" alisisitiza Mungi.

"Aliongeza kwamba, msanii anapotumia mitandao ya kijamii kwa kuweka picha chafu, zisizo na maadili au kitu chochote kisicho na staha ni kuchafua wajihi wake mbele ya jamii na hili linampotezea fursa nyingi za kibiashara na kiuchumi maana hakuna kampuni au asasi itakayopenda kufanya kazi na msanii mwenye sifa mbovu.


"Wasanii wanapotumia hovyo mitandao ya kijamii wanachafua wajihi wao katika jamii. Wanajikosesha fursa za kimapato. Mfano; mfanyabiashara anapotaka kutangaza shule yake ya watoto wa awali hawezi kutumia msanii mwenye wajihi mchafu na unaoharibu watoto" aliongeza Mungy.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Sanaa na Masoko wa BASATA, Vivian Shalua alisema kwamba Baraza hilo muda wote limekuwa likisisitiza maadili mema miongoni mwa wasanii maana vijana wengi huwaangalia kama mfano katika maisha yao.


"Kila mara BASATA limekuwa likisisitiza maadili kwa wasanii wote. Kazi hii ni ngumu na inataka wadau wote kushiriki katika kunyoosha maadili ya wasanii na vijana kwa ujumla" alimalizia Shalua.


Copyright © 2021. All Rights Reserved.