Habari na Matukio

Tarehe: 2/11/2019

WASANII KATIKA FANI YA UCHORAJI WASHAURIWA KUCHORA PICHA ZENYE KUAKISI MAISHA HALISI YA JAMII YETU KIUCHUMI, KIJAMII, MILA NA UTAMADUNI WA MTANZANIANa Mwandishi Wetu

Akifungua Maonyesho ya Sanaa za Ufundi yaliyoandaliwa na Shirika la East Africa Art Biennale(EASTAFAB)katika ukumbi wa Nafasi Arts Space jijini Dar Es Salaam,Mwenyekiti wa bodi ya Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA)Bw.Abby Gunze ambaye alimwakilisha Waziri wa Habari,Utamaduni Sanaa na michezo Dkt.Harrison Mwakyembe,amesema wasanii wanapaswa kujiuliza:


“Ni sanaa yenye ujumbe gani itakayo kueleweka kwenye jamii za enzi hizi?Pia anachora sanaa kwa kwa madhumuni gani?Sanaa ni njia ya mawasiliano kati ya msanii na mtazamaji.Je sanaa yake ina mawasiliano na jamii anamoishi?”
Kwa kutambua umuhimu wa sanaa hapa nchini Tanzania,Mwenyekiti wa Bodi ya BASATA,Bw.Gunze anabainisha kuwa Tanzania inajulikana sana duniani kuwa chanzo cha sanaa za kuchorwa katika miamba, hususani katika maeneo ya Kolo,Kondoa na sehemu za Msighaa pale Singida,hivyo wasanii na jamii nzima ya watanzania, wanapaswa kutambua kuwa sanaa ile iliyochorwa kwenye miamba iliundwa kwa ajili ya jamii zilizoishi wakati ule na kwamba zilizingatia mila na desturi za maisha yao.


Pamoja na kuwapongeza wasanii wote walioshiriki katika maonyesho haya ya Africa Art Biennale(EASTAFAB), Bw.Gunze kama mgeni rasmi pia ametumia fursa hii kuwashukuru wawakilishi wa nchi rafiki za Uswisi,Ujerumani,Ubelgiji,kwa kusaidia kuwepo kwa maonyesho haya.


Naye mwenyekiti wa Kamati ya(EASTAFAB) Prof.Elias Jengo,ameishuru Serikali ya Tanzania kupitia Naraza la Sanaa BASATA wanaofanya kazi zao chini ya Wazara ya Habari,Utamaduni Sanaa na michezo,sambamba na kituo cha wasanii wa Nafasi Arts Space pamoja na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kukuza na kuendelea kazi za Sanaa hapa nchini.


Kwa kutambua thamani ya Sanaa hapa nchini,Prof.Jengo anasema tarehe 6 Novemba 2019 katika kituo cha wasanii wa Nafasi Arts Space kutafanyika kongamano lenye mada ya Utalii na Sanaa litakalo wajumuisha wasanii mbali mbali katika fani za Uchoraji,wanamitindo,wachongaji jinsi wanavyoutizama Utalii katika fani zao.


Nchi zilizoshiriki katika maonyesho ya Sanaa za Ufundi(Fine Arts) yaliyoandaliwa na shirika la East Africa Art Biennale(EASTAFAB) ni pamoja na mwenyeji Tanzania,Kenya,Uganda,Rwanda,pamoja na Burundi.
Copyright © 2021. All Rights Reserved.