Habari na Matukio

TANGAZO KWA WASANII WOTE

Tarehe: 21/04/2016

WADAU WATAKA SIKU YA MSANII IAZIMISHWE NCHI NZIMA

Na Mwandishi Wetu

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye tathmini ya maazimisho ya Siku ya Msanii maarufu kama Msanii Day iliyofanyika mapema wiki hii ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) zilizoko Ilala Sharif Shamba wadau hao walieleza kusikitishwa na siku hiyo muhimu kuadhimishwa mkoa wa Dar es Salaam pekee huku wasanii wa mikoani wakiachwa nyuma.


"Tanzania ina wasanii wengi, haiwezekani siku hii muhimu kwao iwe inagusa wasanii wachache tu. Tunaamini halmashauri na mikoa ina nafasi kubwa ya kuwaunganisha wasanii nchi nzima na kuunga mkono juhudi za Baraza katika kuadhimisha siku hii" alisema Msanii wa Sanaa za Maonesho Nkwama Ballanga.


Aliongeza kuwa kupitia maafisa Utamaduni shughuli za Sanaa zimekuwa zikiendelea maeneo mbalimbali nchini hivyo lazima kuwe na maelekezo maalum kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ya kuwataka maafisa Utamaduni kuwaunganisha wasanii wote katika kuadhimisha siku hii ambayo imekuwa ikiadhimishwa Dunia nzima huku kila nchi ikiwa na namna yake ya kuadhimisha.


Tunajua wasanii katika halmashauri zetu wanafanya kazi nzuri sana lakini pia wana changamoto nyingi zinazowakabili. Kuunga mkono maadhimisho ya siku yao nchi nzima ni kujenga mfumo wa wao kujipongeza, kujitathimi lakini pia kuonesha kazi zao mbalimbali kulingana na fani zao” aliongeza Ballanga.


Kwa upande wake Msanii Ahmad Dadi wa Kundi la Sanaa za Maonesho la Lumumba alisema kuwa siku ya Msanii ni muhimu katika kutambua na kuthamini mchango wa wasanii mbalimbali nchini hivyo lazima kuwe na juhudi za makusudi za kuifanya yenye kufana na yenye kumgusa kila Msanii nchini.


"Tuna wasanii wakongwe ambao wamefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi. Hii ndiyo fursa ya kuwaonesha wasanii wa kizazi cha sasa hali ya Sanaa ilivyokuwa. Kuwepo kwa majukwaa ya maadhimisho kama haya nchi nzima kutaonesha thamani ya Sanaa nay a wasanii" alisema Dadi.


Siku ya Msanii mwaka huu imepangwa kuazimishwa Oktoba 29 ambapo inatarajiwa kupambwa na shamrashamra mbalimbali.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO - BASATACopyright © 2021. All Rights Reserved.