Habari na Matukio


Tarehe: 31/03/2014

WASANII WATAKIWA KUHIFADHI KAZI ZAO, KUMBUKUMBU


Na Mwandishi Wetu

Wasanii nchini wametakiwa kujenga utamaduni wa kuhifadhi kazi zao na kumbukumbu mbalimbali zinazowahusu ili kuepuka kupotea, kusahaulika na kuwezesha kuzirithisha kwa vizazi vijavyo.

Wito huo umetolewa mapema wiki hii na wadau wa Jukwaa la Sanaa linaloandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwenye ukumbi wa Baraza hilo ulioko Ilala Sharif Shamba.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao wa Jukwaa la Sanaa walisema kwamba kumekuwa na tatizo kubwa la wasanii kutokuweka kazi zao katika maandishi na mifumo mbalimbali ya uhifadhi hali ambayo imekuwa ikisababisha kazi zao kupotea, kukosekana kwa kumbukumbu na mbaya zaidi kukata mnyororo wa urithishaji weledi.

"Kuna tatizo kubwa miongoni mwa wasanii katika kuhifadhi kazi zao. Hapa lazima tuseme maana linawagusa hata hao wasanii wakubwa wanaojiona maarufu. Hawahifadhi kazi zao. Mathalan hawaziandiki katika weledi wa muziki" alisema Francis Kaswahili ambaye ni mdau wa Sanaa.


Aliongeza kwamba, msanii yeyote anayekuwa makini katika kazi zake lazima aziweke kazi zake katika kumbukumbu maalum, kama ni muziki ahakikishe umeandikwa katika nota na kiweledi ili uhifadhiwe kwa ajili ya matumizi na kumbukumbu za baadaye.


Aidha, wadau wengi walieleza kwamba taasisi za chama cha hakimiliki na hakishiriki (Cosota) na BASATA kwa pamoja zimekuwa zikiwakumbusha mara zote wasanii kuhifadhi kazi zao lakini bado mwamko umekuwa mdogo miongoni mwao hali inayotishia kupotea kwa kazi zao na kusahaulika moja kwa moja.


Awali akiwasilisha mada katika Jukwaa hilo Mratibu wa miradi wa kundi la Lumumba Art Theatre Muhaza Mwalimu alisema kuwa kundi lao liko kwenye mikakati ya kuanza kuhifadhi kazi zao ambapo kwa sasa limewapeleka wasanii wake wawili katika mafunzo maalum ya uandishi wa muziki na uhifadhi.


Copyright © 2021. All Rights Reserved.