Habari na Matukio

Tarehe: 15/10/2019

BASATA YATAKIWA KUPELEKA MAFUNZO YA BATIKI ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu

Nguo hizi ni nzuri sana tena za kipekee, na utaalamu huu inabidi uendelezwe kwa vijana wetu kote nchini,kwani kupitia utaalamu huu vijana wetu wanaweza kujiajiri wenyewe na hata kuajiri wenzao. Natamani pia mafunzo haya yawafikie pia vijana wetu kule Zanzibar, nashauri utengenezwe mpango maalumu kwa mashirikiano ya pande zote mbili ili kuona ni jinsi gani mafunzo haya yanaweza kuendelezwa na kule Zanzibar.” alisema Mhe. Bi. Mwantatu. Mhe. Bi. Mwantatu aliyasema hayo leo wakati yeye pamoja kamati yake anayoiongoza walipotembelea kwenye moja ya banda la wasanii wanaotengeneza nguo mbalimbali za batiki lililopo ndani ya maeneo ya Basata (Ilala – Shariff Shamba).
Pamoja mabanda ya batiki, pia kamati hiyo ilipata fursa ya kutembelea darasa la mafunzo ya muziki lililopo Baraza na kujionea hatua mbalimbali za uandaaji na utengenezaji wa kazi za muziki pamoja na jinsi ya kutumia vifaa (ala) mbalimbali za muziki. .
Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, leo imelitembelea Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kufanya kikao cha pamoja kwa lengo la kubadilishana uelewa na kuimarisha mahusiano. Ujumbe huo kutoka Zanzibar umeambatana na viongozi mbalimbali kutoka mamlaka nyingine zilizopo Zanzibar kama vile Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Amour Hamil Bakari, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni (BASSFU) Bw. Omar Ali Adam, Katibu Mtendaji wa COSOZA Bi. Mtumwa Khatib Amer, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) Bi. Mwanahija Ali Juma, Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti Bi. Saumu Ali Saidi pamoja na watendaji mbalimbali wa mamlaka hizo.
Katika kikao hicho cha siku moja, wajumbe hao wameeleza uzoefu wao kiutendaji katika maeneo yao kwa lengo kubadilishana uelewa kuhusu kazi na faida ya Sanaa hapa nchini. Mojawapo ya maswala yaliyozungumziwa ni pamoja na maeneo ya usajili, tozo mbalimbali za gharama za usajili, programu mbalimbali zinazosimamiwa na Basata kama vile Sanaa kwa watoto, Mashindano ya ulimbwende, Jukwaa la Sanaa, ujenzi wa ukumbi mpya wa Baraza, usimamizi wa Sanaa Kikanda pamoja na mafunzo mbalimbali yanayosimamiwa na kuratibiwa na Basata, pia ujumbe huo ulitaka kujua mikakati mbalimbali ya Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA) katika kukuza, kuendeleza na kusimamia Sanaa na Wasanii nchini. Mwenyeji wa ujumbe huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa Baraza walipata fursa ya kuelezea majukumu ya BASATA na kuyatolea ufafanuzi baadhi ya maswali na hoja mbalimbali zilizoibuliwa kwenye kikao hicho.
Kwa pamoja kikao hicho kimependekeza kuwe na ratiba maalumu ya kutembeleana kila mwaka ili kuzidi kujifunza na kubadilishana uzoefu zaidi kwani mambo mapya huwa yanazaliwa kila siku katika sekta ya Sanaa. Aidha Bw. Mngereza ametumia pia nafasi hii kupongeza kwa dhati ziara hii na kuahidi kuendeleza mashirikiano haya. “Sisi kama Baraza, tumefarijika sana kupokea ugeni huu mkubwa, wenye lengo kubwa la kukuza pamoja na kuimarisha ustawi wa sekta ya Sanaa na wasanii nchini.tunaahidi kushirikiana vyema kwenye utekelezaji wa mipango yote iliyoazimiwa kwenye kikao hiki, aidha karibu tena na tena kwani hapa pia ni nyumbani kwenu” alimaliza Bw. Mngereza.

Copyright © 2021. All Rights Reserved.