Parliament Logo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Baraza la Sanaa la Taifa

BASATA na TRA waungana kuwatambua Manju Muziki (DJ...

22 Jan, 2026
BASATA na TRA waungana kuwatambua Manju Muziki (DJ’s)

Isack N. Bilali

Zaidi ya manju muziki (DJ’s) 100 wamehudhuria mafunzo ya urasimishaji na elimu ya mlipa kodi yaliyoandaliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yaliyofanyika tarehe 20 Januari 2026 katika viwanja vya Hekima Garden, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo ni sehemu ya kampeni endelevu ya BASATA ya kurasimisha shughuli za sanaa nchini, yakilenga kuwafikia DJ’s katika wilaya na mikoa yote ili kufanya kazi zao kwa misingi ya kisheria, kupanua fursa na kulinda thamani ya kazi zao.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Sanaa Mwandamizi wa BASATA, Bwana Abel Ndaga, amesema urasimishaji utasaidia kukomesha manyanyaso kwa DJ’s yanayotokana na kukosekana kwa mikataba rasmi. Ameeleza kuwa BASATA imeandaa mkataba wa kazi utakaotumiwa na DJ’s waliosajiliwa ili kuhakikisha makubaliano halali wanapopata kazi.

Ameongeza kuwa urasimishaji unafungua fursa mbalimbali ikiwemo mikopo kupitia Mfuko wa Utamaduni, ambao unapatikana kwa wadau waliorasimishwa. Baadhi ya DJ’s maarufu kama Ali B wamenufaika tayari na mfuko huo. Pia, BASATA hutoa msaada wa kisheria bila malipo kupitia kitengo chake cha sheria chenye mawakili wabobezi.

Kuhusu usajili, Ndaga amesema DJ’s wanaweza kujisajili kwa urahisi popote walipo kupitia tovuti ya sanaa.go.tz, wakihitaji namba ya TIN na kitambulisho cha NIDA.

Kwa upande wao, DJ’s wameishukuru Serikali kwa juhudi za kuwatambua na kuwawekea mazingira bora ya kukuza sekta bunifu. DJ Smah ameomba Serikali izingatie kupunguza gharama za kodi kwenye uingizaji wa vifaa vya kazi vinavyotoka nje ili kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na kuongeza ushindani na ubunifu katika sekta hiyo.

Settings