Isack Bilali, BASATA.
Naibu Katibu Mkuu Dkt. Suleman Serera ameagiza Baraza la Sanaa la Taifa kusimamia suala la maadili kuanzia ngazi ya msingi ili kuepuka madhara katika jamii na kizazi kijacho.
Ameyasema hayo leo tarehe 24 Aprili, 2024 jijini Dar es salaam alipotembelea na kuongea na menejimenti ya Baraza huku akiweka wazi kuwa sanaa ina ushawishi mkubwa kuhamasisha jamii na kuijenga vile inavyotaka.
Naibu Katibu Mkuu ameongeza kuwa, Baraza la sanaa lifuatilie kwa karibu na ufanisi juu ya namna bora ya kuimba wimbo wa Taifa na uzalendo kwa usahihi, kwakuwa ameshashuhudia wengi wakikosea matamshi katika baadhi ya maneno yaliyomo katika wimbo wa Taifa hivyo kuharibu mantiki.
“Baraza linapaswa kufuatilia na kuweka utaratibu wa namna kuimba nyimbo za Taifa na uzalendo iwe kwa kufundisha au kutoa elimu ilimradi kujenga utamaduni kwa wananchi wawe na uwezo na uelewa wa nyimbo zao” amesisitiza Dkt. Serera.
Ameenda mbali zaidi kwa kutolea mfano baadhi ya maneno ambayo yanakosewa na baadhi ya wananchi wakati wa uimbaji wa wimbo wa Taifa ni pale wanapochanganya badala ya kutamka neno “hekima” wengi wao wanakosea na kutamka neno “heshima” jambo ambalo siyo sahihi.
Makosa mengine ambayo yamebainishwa na kukemewa ni pamoja na namna ya uimbaji kutokana na kuibuka baadhi ya watu au kundi kupendelea kuimba kupitia rekodi pamoja na wengine kutozingatia umuhimu wa kuimba na kumaliza beti zote mbili kwa ufanisi.
Baraza la Sanaa la Taifa limepokea na kuhakikisha litafanya utekelezaji wa kuhamasisha kwenye vyombo vya habari na kutembelea makundi mbalimbali ikiwemo kuimarisha mafunzo katika programu ya sanaa kwa watoto ili wale walio shule waendelee kuwa mabalozi wa uzalendo.