Isack Bilali, BASATA.
Mrembo wa Tanzania 2022 Halima Kopwe ambaye ameiwakilisha nchi katika mashindano ya urembo duniani ametinga katika hatua ya kumi bora kupitia kipengele cha “Beauty with purpose project” kwenye shindano hilo lililofanyika nchini India ambapo kila mshiriki alipaswa kuwasilisha mradi unaoleta matokeo chanya kwa jamii.
Halima ametinga katika hatua hiyo kufuatiwa na kampeni yake ya “Damu yangu, Kizazi Changu” mradi ambao umelenga kuboresha afya kwa wanawake wajawazito na watoto nchini Tanzania ambao utasaidia kupunguza vifo kwa mama na mtoto.
Aidha ukiachilia mbali kupunguza vifo kwa mama na mtoto mradi huo pia umelenga kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuchangia damu pamoja na kukusanya fedha kusaidia vifaa vya matibabu na kutoa bima kwa watoto wenye uhitaji.
Alipoulizwa sababu ya kuchagua kundi hilo la mama na mtoto, mrembo huyo ameweka wazi kuwa msingi wa ustawi na makuzi bora katika jamii unaanzia kwenye kundi hilo lenye uhitaji mkubwa hivyo ukiligusa kimkakati unakuwa umefanikiwa kujenga jamii bora, makini yenye uthubutu na uhakika wa kujiendeleza.
Ikumbukwe kuwa shindano la urembo la dunia lililofanyika kuanzia Februari 18, 2024 na kilele chake kufanyika Machi 9, 2024 nchini India lilikuwa la msimu wa 71 wa shindano hilo ambapo jumla ya washiriki 120 kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania iliyowakilishwa na Halima Kopwe wametumia siku 21 kufanya mashindano mbalimbali na shughuli za hisani ili kuweza kumpata mrembo mmoja aliyetwazwa kuwa Mrembo wa Dunia.
ukifuatilia historia ya shindano hilo bara la Afrika imewahi kutoa mshindi mara tano kupitia nchi tatu yaani Misri, Afrika ya kusini na Nigeria ambapo kwa Afrika kusini ilishinda taji hilo mwaka 1958, 1974 na 2014, upande wa Nigeria hao walishinda taji hilo mwaka 2001 huku Misri wakilitwaa mwaka 1954.
Katika mahojiano yake mara baada ya kurejea kutoka kwenye shindano hilo Halima ameishukuru Serikali kupitia Baraza la sanaa la Taifa kwa ushirikiano ambao umempa hamasa ya kuitangaza nchi kupitia kipengele cha “Beauty with purpose project” alipoingia 10 bora na kuwapiku washiriki kutoka nchi 71 jambo ambalo ameahidi kutoa ushirikiano kwa warembo wengine ili waweze kupata nafasi ya juu zaidi.