
Mwanamuziki wa Hip Hop; Kutoka Tanga Hadi Umaarufu Afrika Mashariki
Utangulizi
William Nicholaus Lyimo, anayejulikana zaidi kwa jina la kisanii Bill Nass, ni msanii wa muziki wa hip hop kutoka Tanzania aliyezaliwa tarehe 11 Aprili 1993 katika Mkoa wa Tanga. Msanii huyu mwenye asili ya Kichagga amejijengea heshima kubwa ndani na nje ya Tanzania kupitia vipaji vyake vya muziki, ubunifu na ushawishi mkubwa katika jamii ya vijana.
Mnamo mwaka 2017, kituo cha kimataifa cha MTV Base kilimtaja miongoni mwa wasanii “50 Artists To Watch For” jambo lililomweka kwenye ramani ya kimataifa. Hadi sasa, Bill Nass anaendelea kuwa miongoni mwa nyota wakubwa wa muziki wa kizazi kipya nchini na barani Afrika.
Maisha ya Awali na Elimu
Bill Nass alizaliwa katika Hospitali ya Bombo, Tanga na wazazi wake ni wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro. Safari yake ya elimu ilianzia Shule ya Msingi Mbuyuni (2000–2003), kisha Shule ya Msingi Mkunguni jijini Dar es Salaam. Alisoma Katika Sekondari ya Oysterbay (2007–2010), kisha kuendelea na masomo ya juu katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ambapo alihitimu Shahada ya Ununuzi na Ugavi (2017).
Safari ya Muziki
Bill Nass alianza kupata umaarufu mwaka 2014 baada ya kuachia wimbo wake wa kwanza “Raha”. Mwaka uliofuata, aliteuliwa kwenye Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA 2015) kama msanii bora chipukizi.
Mwaka 2017 ulikuwa wa kipekee kwake baada ya kushiriki katika Coke Studio Africa kama msanii wa “Big Breakthrough Artist” ambapo alitumbuiza pamoja na wasanii kutoka Uganda na Ethiopia. Aidha, ameshiriki kwenye majukwaa makubwa ya muziki nchini ikiwemo Fiesta na Wasafi Festival.
Mwaka 2021, Bill Nass alianzisha Mafioso Inc., lebo yake ya muziki na kufanikiwa kutoa ngoma zilizotikisa kama “Puuh” akimshirikisha Jay Melody, wimbo ulioongoza chati za Boomplay kwa wiki sita mfululizo na kuvunja rekodi kwa zaidi ya milioni 51 za wasikilizaji mtandaoni.
Mnamo 2022, alinyakua tuzo ya Msanii Bora wa Hip Hop (Tanzania Music Awards) na mwaka 2025 akatangazwa Msanii Bora wa Hip Hop Afrika Mashariki (EAEA Awards) akiwashinda wanamuziki wakubwa kutoka Kenya, Uganda na Rwanda.
Mradi wa Kijamii: Chuo kwa Chuo
Mwaka 2024, Bill Nass alizindua kampeni ya vijana iitwayo “Chuo kwa Chuo”. Mradi huu ulijikita katika kutembelea vyuo na taasisi mbalimbali nchini kwa ajili ya burudani, mashindano ya vipaji na mijadala ya kielimu kuhusu masuala ya afya ya akili na ujasiriamali.
Licha ya changamoto ndogo zilizojitokeza, ikiwemo mjadala mkali baada ya tukio katika Chuo cha TIA Dar es Salaam, mpango huu ulipongezwa kwa ubunifu na mchango wake katika kuwaunganisha vijana kupitia muziki, elimu na utamaduni.
Maisha Binafsi
Majina halisi ya Bill Nass na majina halisi ya Faustina Charles Mfinanga (Nandy). Wawili hawa ni baadhi ya wasanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania, na safari yao ya maisha binafsi imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na mashabiki kutokana na uhusiano wao wa kimapenzi.
Mwaka 2020, uhusiano wao ulionekana kuwa thabiti zaidi na walianza kushirikiana kwa karibu zaidi katika maisha binafsi na kazi zao za kisanii. Baada ya kipindi cha uhusiano wa kudumu na mshikamano thabiti, waliufanya uhusiano wao rasmi kwa kufunga ndoa mwaka 2022. Hadi sasa, wanajulikana kuwa na mtoto mmoja na wakiwa mstari wa mbele katika muziki wa Tanzania, wanasalia mfano wa mshikamano, upendo na ushirikiano wa kisanii.
Mbali na muziki, Billnass ametumia taaluma yake ya Biashara kutoka CBE kuanzisha kampuni ya vifaa vya kielektroniki, Nenga Tronix, mwaka 2021. Kampuni hii inauza bidhaa za kisasa kama simu, kompyuta na vifaa vya nyumbani, kwa lengo la kutoa huduma bora, bidhaa zenye ubora na bei nafuu, sambamba na kukuza ajira kupitia ujasiriamali.
Tuzo na Mafanikio
- KTMA 2015 – Msanii Bora Chipukizi (nominated)
- Tanzania Music Awards 2022 – Msanii Bora wa Hip Hop
- EAEA Awards 2025 – Msanii Bora wa Hip Hop Afrika Mashariki
Kwa zaidi ya muongo mmoja, Bill Nass ameendelea kuwa chachu ya maendeleo ya muziki wa hip hop nchini Tanzania. Uwezo wake wa kuunganisha muziki, elimu, na uhamasishaji wa kijamii umemfanya kuwa mfano bora wa kuigwa na vijana wengi. Kupitia kazi zake na miradi yake ya kijamii, amethibitisha kuwa sanaa ni zaidi ya Burudani ni chombo cha mabadiliko, biashara, na daraja la kuunganisha jamii.