Isack Bilali, BASATA.
Mkurugenzi wa idara ya ukuzaji na maendeleo ya sanaa BASATA bwana Edward Buganga ameipongeza kampuni ya “Kilimanjaro one travel and tours” kwa kuwezesha waandaaji wa tamasha la “lake zone cultural and tourism festival” ambalo kimsingi limelenga kudumisha na kurithisha misingi ya utamaduni wa Kitanzania.
Ameyasema hayo wakati anaongea na waandishi wa Habari katika hafla fupi ya uzinduzi wa tamasha hilo katika ukumbi wa hoteli ya serena jijini Dar es salaam tarehe 07 Juni, 2024 ambapo tamasha hilo litafanyika katika wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kuanzia tarehe 5 hadi 7 Julai mwaka huu.
Aidha, mkurugenzi ameihakikishia kampuni hiyo kuwa itapata ushirikiano wa kutosha kutoka serikalini hususani wataalam wa Baraza ambao wanasimamia ukuzaji wa maendeleo ya sekta ya sanaa nchini kwa kushirikiana na wadau kama wao ambao kimsingi wamekuwa mstari wa mbele katika ushirikiano kuanzia hatua za awali hadi sasa.
Kwa upande wa waandaaji wa tamasha hilo wameweka bayana kuwa wanachokifanya ni kuunga mkono serikali ya awamu ya sita katika juhudi zinazooneshwa hususani uwekezaji kwenye sekta ya sanaa hivyo ni wajibu wao kudumisha uzalendo, umoja wa kitaifa kwakuwa utamaduni ni kielelezo cha utaifa.