
Watumishi "BASATA" kuboresha msingi wa utoaji huduma kwa wadau
Isack N. Bilali, BASATA.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi Baraza la sanaa la Taifa Ndugu Mgunga A. Mwamnyenyelwa (mjumbe wa Bodi) amewahimiza watumishi wa Baraza kuendelea kuwa wabunifu kipindi wanapokutana na kutoa huduma kwa wadau wa sanaa ambao kwa kiasi kikubwa Baraza ndiyo chombo chao kinachoshughulikia masuala yote yanayohusu kazi zao, kwa kufanya hivyo itajenga na kuimarisha uhusiano wenye kujenga taswira imara baina ya Serikali na wadau wanaonufaika katika sekta ya sanaa nchini.
Ameyasema hayo wakati hotuba yake ya ufunguzi katika mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Baraza hilo kwaajili ya kuwajengea uwezo watumishi wake katika eneo la utoaji wa huduma kwa wateja yanayofanyika katika ukumbi wa TAMISEMI Kivukoni jijini Dar es salaam kuanzia tarehe 17 hadi 18 Machi, 2025 ambapo kila mtumishi anatarajiwa kuwa balozi wa kutangaza na kutetea sekta ya sanaa ambayo imeonesha kukua kwa kiasi kikubwa hivyo kuwa moja ya nguzo muhimu katika kuingiza kipato kwa wadau wake na nchi kwa ujumla.
Mgeni rasmi ameendelea kusema kuwa, kwa kiasi kikubwa serikali ya awamu ya sita imeonesha nia thabiti katika kuimarisha mifumo ya maenedeleo ya sekta ya sanaa kwahiyo jukumu limebaki kwa wasimamizi kutafsiri kwa usahihi sera na maelekezo yanayotolewa na serikali ili yaaweze kuwafikia kwa usahihi wasanii na wadau wa sanaa kabla ya wao kujitafsiria wenyewe kwani ikitokea kufanyika hivyo watatokea watu ambao watatoa tafsiri potofu itakayopoteza maana mzima ya lengo lililoazimiwa, ambapo watu wenye jukumu la kufanya hivyo ni Baraza, hivyo mafunzo yanayofanyika ni ya msingi sana kwa kila mtumishi kuhakikisha anaelewa ili kufanikisha hadhma ya utoaji huduma bora kwa wateja.
Baraza la sanaa la Taifa limeazimia kujikita katika kutoa na kusimamia shughuli za sanaa katika falsafa ya kuwaonesha wasanii na wadau wa sanaa kuwa "Sanaa ni Biashara, Uchumi na Ajira" ili kila mwenye ujuzi katika sanaa aweze kufanya shughuli zake akiwa rasmi kwa minajili ya kujipatia kipato chake lakini kutenegeneza nafasi kwa watu wengine kunufaika na shughuli za sanaa jambo ambalo litasaidia kuinua uchumi wa nchi, pamoja na yote wasanii na wadau wa sanaa wanhimizwa kujisajili baraza ili wawe rasmi na kukutana na fursa zilizopo kupitia mfumo wa AMIS unaopatikana katika kiungo cha sanaa.go.tz